WAZIRI
MKUU Kassim Majaliwa amewataka wakuu wa mikoa 11 inayolima pamba nchini
wahakikishe wanasimamia vizuri wakulima wa zao hilo ili kuongeza
uzalishaji na kuwaletea tija wananchi.
Agizo
hilo limetolewa Jumanne, Septemba 26, 2017 na Waziri Mkuu wakati
akizungumza na wakuu hao wa mikoa kwenye kikao alichokitiisha mjini Dar
es Salaam kujadili maendeleo ya zao hilo.
Kikao hicho ni muendelezo wa kikao alichokitiisha mjini Dodoma (Ijumaa, Septemba 8, 2017) kujadili mbinu za kufufua zao hilo.
Wakuu
wa mikoa walioitwa kwenye kikao hicho ni kutoka mikoa ya Shinyanga,
Singida, Kagera, Tabora, Morogoro, Mara, Mwanza, Simiyu, Katavi, Kigoma
na Geita.
Waziri
Mkuu amesema katika kipindi hiki ambacho msimu wa maandalizi ya kilimo
cha pamba umeanza ni vema kwa Maofisa Kilimo na Wagani wakawasimamia
wakulima kwa ukaribu ili wahakikishe wanafuata mbinu bora za kilimo.
Amesema
iwapo wakulima watapata usimamizi mzuri kutoka kwa Maofisa Ugani
waliopo kwenye maeneo yao kuanzia hatua za awali za utayarishaji wa
mashamba yao itawasaidia katika kuongeza tija, kwenye uzalishaji wao.
“Serikali
inawataka Maofisa Kilimo na Wagani wawasimamie wakulima kuanzia
maandalizi ya shamba, kupanda, matumizi ya pembejeo na dawa, kuvuna na
kutafuta masoko ili kilimo cha zao hilo kiweze kuwaongezea tija.”
Amesema
Maafisa Kilimo wote walioko kwenye kila Halmashauri ni lazima wahusike
kikamilifu katika kuwaelekeza wakulima namna ya kutumia mbinu bora za
kilimo ili waweze kupata mazao mengi , hivyo kujikwamua kiuchumi.
Pia
Waziri Mkuu amewaagiza Wakuu wa Vyuo vya Kilimo nchini wahakikisha
wanakuwa na mashamba darasa yatakayotumika na wakulima na wanafunzi wao
kujifunza mbinu bora za kilimo kwa vitendo.
Kikao
hicho kilihudhuriwa na Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi, Dkt. Charles
Tizeba; Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais – TAMISEMI; Bw. Suleiman
Jafo, Makatibu Wakuu wa Ofisi ya Waziri Mkuu na Wizara ya Kilimo, Mrajis
wa Vyama vya Ushirika nchini, Dkt. Tito Haule na Mkurugenzi
Uhamasishaji Mazao, Bw. Twahir Nzallawahe.
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU.
Comments
Post a Comment