Waziri Ndalichako Aanika MADUDU Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB)

Serikali  imeeleza kwamba matatizo ya Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB) ni kulipwa kwa wanafunzi hewa, ubadhirifu wa fedha na kuwepo kwa watendaji wanaohusika kuweka fedha za wanafunzi wanne kwa mwanafunzi mmoja.

Kadhalika imeeleza tabia ya HESLB kujiona ‘Mungumtu’, kuwaona watoto wa Watanzania kama ni shida kwao na wasiostahili kupewa mikopo na hata kuwa na majibu ya mkato yasiyokuwa na chembe ya kazi ya utoaji huduma. 

Waziri wa Elimu, Sayansi ya Teknolojia, Profesa Joyce Ndalichako  alisema hayo jana jijini Dar es Salaam wakati akizindua Bodi mpya ya HESLB na kuitaka kujitenga na menejimenti wakati wa utekelezaji wa majukumu yake na kuhakikisha matatizo hayo yote ambayo yapo katika taarifa aliyowakabidhi, yanakaguliwa upya, kuhakikiwa na kufanyiwa kazi.

Pia alisema taarifa hiyo imeambatanisha taarifa ya fedha za HESLB zilizochezewa. 

Alikabidhi taarifa hiyo kwa Makamu Mwenyekiti wa bodi mpya, Madina Mwinyi akiagiza ifanyiwe kazi kuhakikisha na kujiridhisha pamoja na kuwajua wadeni wa HESLB huku ikiepuka kuiamini menejimenti kama ilivyokuwa kwa bodi ya awali badala yake kuisimamia. 

“Ninakabidhi taarifa yenye changamoto za Bodi ya Mikopo kwenu Bodi ya Wakurugenzi ambayo inaainisha uwepo wa wanafunzi hewa na ambao wanalipwa mikopo wakiwemo waliomaliza au kuacha chuo,” alisema.

Pia alisema taarifa hiyo inahusisha kuwepo kwa watendaji wanaohitajika kujieleza ambao walikuwa wakiweka fedha za wanafunzi wanne kwa mwanafunzi mmoja ambapo ushahidi upo na eneo hilo bado kuna shida. 

Kadhalika, aliiagiza Bodi mpya kutazama upya na kujiridhisha kuhusu vigezo vya utoaji mikopo kwani kumekuwa na matatizo, na hata kutizama utoaji wa mikopo kama taratibu na sheria zinazingatiwa. 

“Malalamiko ya Bodi ya Mikopo yapunguzwe ama kuondolewa kabisa ili kukidhi matarajio ya wadau wa elimu nchini, endeleeni kukagua na hata majina ya wanaohitajika kupata mikopo kabla ya kutolewa rasmi,” alisema Profesa Ndalichako.

Kuhusu Bodi mpya aliitaka isimamie zaidi urejeshwaji wa mikopo kwani hadi sasa serikali imetoa Sh trilioni 3.1 tangu kuanzishwa kwa bodi, lakini ni Sh milioni 217 pekee zilizorejeshwa huku Sh bilioni 588 zikiwa zimefikia muda wake zikitakiwa kulipwa.

 Akizungumza baada ya bodi hiyo kuzinduliwa, Makamu Mwenyekiti, Madina Mwinyi alisema katika kufanyia kazi changamoto za HESLB wataanza kwa kujipanga wao wenyewe katika taasisi wanamotoka ili kila mmoja kujua ni kiwango gani cha mikopo kinachotakiwa kurejeshwa.

Kadhalika alisema bodi hiyo itahuisha taswira ya HESLB pamoja na kuiaminisha jamii kuwa suala la mkopo wa elimu ya juu ni lazima kurejeshwa kwa wakati. 

Wajumbe wa bodi hiyo na taasisi wanazotoka katika mabano ni Profesa Caroline Nondo (Mwakilishi kutoka Tume ya Vyuo Vikuu), Susan Urio (Mwakilishi wa Wanafunzi), Madina Mwinyi ambaye ni Makamu Mwenyekiti (Mwakilishi wa Wizara ya Elimu Zanzibar).

Wengine ni pamoja na Naibu Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Gerson Mdemu (Mwakilishi wa Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali), Dk Dalmas Nyaoro (Mwakilishi wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia), Frank Mgeta (Mwakilishi wa Wizara ya Fedha na Mipango), Dk Francis Masika (Mwakilishi wa Baraza la Elimu ya Ufundi) na Mjumbe mmoja ambaye ni Mwakilishi wa Wizara ya Fedha Zanzibar hajateuliwa.

Comments